WAKANDARASI NA SEKTA BINAFSI KUWENI WAAMINIFU KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI -
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wakandarasi na Taasisi nyingine za sekta binafsi kuzingatia weledi, maadili na uaminifu katika majukumu yao ili wanapotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iweze kuleta tija kwenye maisha ya Watanzania.
Amesema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi nchini. “Sekta binafsi imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, viwanda sanaa, mawasiliano pamoja na utalii”.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Desemba 11, 2021) alipofungua mkutano wa 21 wa Wanachama wa TPSF na kongamano la biashara na uwekezaji, katika ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mkoani Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuishirikisha sekta binafsi katika ziara za Serikali nje ya nchi kama alivyofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara za nchi za Kenya, Burundi, Marekani, Malawi, Msumbiji na Uganda.
“Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania kupitia utengenezaji wa ajira, kukuza kipato cha wananchi, kutengeneza bidhaa, kuongeza pato la Taifa na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea”.
“Sekta binafsi endeleeni kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati, pamoja na kuhakikisha mnawekeza katika maeneo ya vijijini kwa kuanzisha viwanda katika maeneo hayo ili kupunguza idadi ya watu wanaosafiri kuja maeneo ya mjini kutafuta ajira”
“Nitoe wito kwenu kuendelea kuwaita wawekezaji, kuja hapa nchini na kuwekeza katika sekta mbalimbali za kilimo, utalii na nishati”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuondoa na kupunguza kodi, ushuru na tozo mbalimbali zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji kupitia Sheria za Fedha kwa vipindi tofauti.
“Katika kuzingatia hayo Serikali imepunguza kodi ya sukari ya viwandani kutoka 15% hadi 5%, tozo ya ujuzi kutoka 4.5% hadi 4%; kuwekwa kwa tozo za kulinda viwanda vya Tanzania pamoja na Kodi ya Forodha ya mafuta ghafi ya chakula ambayo imeongezwa maradufu ili kuimarisha ushindani na kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini”.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kutoa wito kwa sekta binafsi kupanua wigo wa uwekezaji katika kuongeza thamani za bidhaa ikiwemo bidhaa za madini, kilimo, misitu, uvuvi na mifugo. Sambamba na kuwekeza katika uzalishaji wa mashine na teknolojia nafuu za urutubushaji vyakula pamoja na uzalishaji wa virutubishi nchini.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mheshimiwa Geoffrey Mwambe amesema licha ya uwekezaji kuendelea kukua nchini Watanzania wameendelea kuwa wadau muhimu kwani hadi sasa usajili wa zaidi ya asilimia 43% uliosajiliwa ni wa wawekezaji wazawa.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda tayari imepeleka mapendekezo ya kuanzisha Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kila halmashauri ili kuongeza ufanisi na kutengeneza mazingira bora ya kiutendaji na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji kuanzia ngazi ya chini.
“ mapendekezo haya tayari yamepita kwenye ngazi ya Makatibu Wakuu na tunasubiri hatua za mwisho za uidhinishaji ili idara hizo zianze”
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amesema licha ya Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, itaendelea kuhakikisha kunakuwa na taasisi imara katika kuwasaidia wawekezaji pamoja na kuboresha Sera za Uwekezaji na Biashara nchini ili kupata Sera nzuri ambazo zinarahisisha biashara na uwekezaji.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF Bi. Angelina Ngalula, kwa niaba ya Sekta Binafsi alitoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita kwa jinsi ilivyoboresha ushirikiano na Sekta binafsi sambamba na kuboresha mazingira na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na kuimarisha mahusiano na nchi za nje.
“Tayari jitihada za kuboresha mahusiano na nchi za nje zimeanza kuzaa matunda na katika kipindi kifupi kumekuwa na mafanikio makubwa kwani uwekezaji kutoka nchi ambazo Rais amezitembelea umeweza kuongezeka”.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, DESEMBA 11, 2021.