KIKAO CHA TAASISI YA SEKTA BINAFSI TANZANIA (TPSF) NA WADAU WA SEKTA YA USAFIRISHAJI NA UCHUKUZI

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambaye pia ni mwakilishi wa kongani (cluster) ya usafirishaji na uchukuzi Bi. Angelina Ngalula, jana tarehe 26-05-2022 aliongoza kikao cha wadau wa Sekta Binafsi wa sekta ya uchukuzi kujadiliana mwenendo wa maendeleo ya Sekta hiyo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau ambao ni wamiliki wa bandari kavu, wasafirishaji wa mizigo, wamiliki wa malori, kampuni za utoaji wa mizigo bandarini, wamiliki na waendeshaji wa maeneo ya kuhudumia mizigo ya export (CFS), kampuni ya meli na waendesha reli binafsi (Private Rail operators).

Kikao hicho Pamoja na mambo mengine mengi yaliyojadiliwa kimeangazia changamoto za usafirishaji zilizosababishwa na Uviko­­-19 na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na lockdown inayoendelea kwenye mji wa Shangai China ambao ni kiunganishi muhimu cha usafirishaji duniani.

Wadau walizungumzia mwendendo wa sekta katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia kutokana na vita inayoendelea baina ya nchi ya Ukraine na Urusi , na matarajio ya sekta baada ya nchi ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wadau pia wameipongeza Serikali kwa hatua na maboresho yaliyofanyika katika sekta ndani ya muda mfupi ambapo wameyataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita.

Mafanikio hayo ni Pamoja na;

 1. Kupunguza msongamano wa meli zilizokuwa zinasubiri kushusha mzigo bandarini kutoka siku 25 hadi siku 0-2.Kwa sasa meli zinashusha moja kwa moja zinapofika bandarini na hakuna kusubiri tena.
 2. Hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kupunguza makali ya bei ya mafuta kwa kutenga bil 100.Hatua hiyo itawezesha sekta ya usafirishaji kuweza kutoa huduma kwa gharama zinazohimilika na kuifanya bandari yetu kuwa shindani, Pamoja na kupunguza gharama za chakula ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea magari makubwa kusafirishwa.
 3. Kuondoa msongamano katika barabara ya kuingia bandarini (Bandari road) pamoja na kutenga eneno kwa ajili ya maegesho ya magari kumerahisisha magari ya mizigo kuingia na kutoka bandarini kwa urahisi.
 4. Hatua za kisera zilizochukuliwa na Serikali pamoja na uwezeshaji unaofanywa na mamlakaya mapato TRA kupitia kitengo cha forodha na Mkemia Mkuu ambapo umewezesha meli kubwa za sulphur inayokwenda nchi za DRC na Zambia kupita kwenye bandari ya Daresalaam. Kwasasa meli zinazobeba tani 20,000 mpaka 40,000 zinahudumiwa katika bandari ya Daresalaam , ambapo meli moja tu inaiingizia Sekta kiwango cha billion 10 kwa meli ya tani 40,000. Hatua hii imesaidia mzigo katika bandari ya Dar eslsalaam kuongezeka na kutoa fursa kwa wasafirishaji wa Tanzania na mnyororo mzima wa usafirishaji kunufaika na hivyo kuendelea kuchangia katika uchumi wa nchi na kuongeza ajira.
 5. Kuruhusu mizigo inayokwenda nje kupelekwa kwenye bandari kavu ili kupunguza msongamano wa mizigo bandarini
 6. Kufunguliwa kwa ofisi ya Ubalozi mdogo katika mji wa kibiashara Lubumbashi. Hatua hii itasaidia katika kuendeleza mahusiano ya kibiashara na kutatuliwa kwa changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza
 7. Kupunguzwa kwa mizani ya kupima magari makubwa barabarani kumesaidia magari kusafiri kwa haraka

Wadau pia walijadili changamoto mpya zilizojotokeza katika kipindi hiki ambazo zinahitaji kutatuliwa ili sekta iweze kukua na kunufaika na ongezeko la shehena. Wadau pia wametoa ushauri katika maeneo hayo

 1. Bandari kavu (ICD) ambazo ziko 13 zenye uwezo wa kuhifadhi containers 27,150 zimezidiwa na mizigo kutokana na ongezeko la mizigo ya transit ambayo zinapangiwa kutokana na ufinyu wa nafasi na vitendea kazi, na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa kuhamisha mizigo kutoka bandarini baada ya meli kushusha mizigo hiyo.
 2. Msongamano wa magari kwenye mpaka wa Kasumbalesa DRC
 3. Migomo ya madereva ambayo inaendelea kwenye makampuni mbalimbali
 4. Gharama kubwa za tozo za makontena ( demurrage charges) zinazotozwa na wenye meli kutokana na ucheleweshaji wa kurejesha makontena. Changamoto hii husababishwa na tatizo la ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo bandarini uliokuwepo kipindi cha nyuma, msongamano wa magari katika mpaka wa Kasumbalesa-DRC pamoja mgomo wa madereva.
 5. Upungufu wa makontena kwa ajili ya kusafirishia makontena pamoja na gharama za kusafirishia makontena (freight rate) kupanda.

MAAZIMIO

Mwisho, kikao kilikubaliana na kuazimia kutatua changamoto zinahusu wamiliki wa meli ikiwemo ya gharama za tozo ya makontena (demurrage charges) kwa kuitisha kikao baina ya kamati ya wadau wa Sekta Binafsi iliyoundwa kupitia kikao hicho na wamiliki wa meli (shipping lines) ili kujadili changamoto hizo. Endapo itashindikana kupata muafaka, swala hilo litapelekwa kwenye mamlaka husika.

Wadau pia wameshauri na kukubaliana changamoto zinazohitaji maamuzi ya Serikali ziwasilishwe na zijadiliwe kupitia Ministerial -Private Dialogues.

Kuhusu changamoto ya madereva, wadau wameazimia swala hili liwasilishwe kwenye kamati ya kushughulikia kero za usafiri na usafirishaji iliyoundwa na Mh. Waziri Mkuu miaka sita iliyopita, yenye wajumbe kutoka vyama vya wamiliki wa malori, wasafirishaji, vyama vya madereva, Wizara ya kazi, Wizara ya uchukuzi, Wizara ya mambo ya ndani, na Wizara ya mambo ya nje.