“Mapitio ya Sera Ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996” Wito wa Kupata Maoni Kutoka kwa Umma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) inafanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996. Sera hii ilitungwa ikiwa ni sehemu mojawapo ya jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili nchi katika kufikia matumizi bora ya rasilimali zake ili kuwezesha kunufaika na kufikia malengo yake ya kiuchumi na ya kijamii. Mapitio haya yanafanyika kutokana na mabadiliko mbalimbali ya mazingira ya biashara na uwekezaji katika ngazi za kitaifa, kikanda na kidunia tangu kutungwa kwa Sera hiyo mwaka 1996. Aidha, mapitio haya pia yatawezesha kutungwa kwa sera mpya ya uwekezaji na kuandaa mkakati wa utekelezaji utakaowezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwa haraka na kutumia ipasavyo fursa zitakazotokana na uchumi wa kati. Vile vile, kazi hii inazingatia dhana ya uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote muhimu.


Hivyo, Serikali inatoa wito kwa umma kuwasilisha maoni na mapendekezo yao ili kufanikisha zoezi hii. Maoni yatakayotolewa yatakua siri na yatatumika kwa ajili ya kufanikisha malengo ya zoezi hili pekee. Maoni yatumwe kabla ya tarehe 20 Septemba 2019 kupitia barua pepe: investmentpolicy@pmo.go.tz au njia ya Posta kwa: Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) S.L.P 980, Mji wa Serikali, Mtumba, DODOMA.

Maoni yanaweza kuhusisha maeneo yafuatayo:


  1. Matumizi bora ya rasilimili za nchi
  2. Upatikanaji wa rasilimali fedha na mitaji kutoka ndani na nje ya nchi
  3. Upatikanaji wa miundombinu wezeshi ya uwekezaji (Maji, Umeme, Nishati n.k)
  4. Kuimarisha ushindani wa mauzo ya nje ya nchi
  5. Mifumo ya kitaasisi yakuwezesha na kukuza uwekezaji
  6. Upatikanaji na umiliki wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji
  7. Mifumo ya kudhibiti wa biashara na uwekezaji
  8. Maendeleo ya Rasilimali Watu
  9. Maendeleo ya Teknolojia na matumizi yake
  10. Vivutio vya Uwekezaji
  11. Mifumo ya kisheria ya kuwezesha na kukuza uwekezaji
  12. Mikataba ya kimataifa ya uwekezaji
  13. Mifumo ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji

“IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, OFISI YA WAZIRI MKUU

(SERA, URATIBU NA BUNGE)

TAREHE 2 SEPTEMBA 2019”