MCHANGO WA SEKTA BINAFSI KUELEKEA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Taaasisi Ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Paul Makanza amesema kua sekta binafsi iko tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha zoezi la sensa ya watu na makazi 2022 linakamilika.

Mr Makanza ameyasema haya Tarehe 15 Agosti katika Mkutano maalumu baina ya Serikali na Sekta binafsi ulio fanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Mkutano huu uliandaliwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya TPSF, Ofisi ya Waziri mkuu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Mgeni rasmi wa mkutano huu alikua Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa (MB).

Akizungumza katika mkutano huu, Bw. Makanza alisema kuwa sekta binafsi iko tayari kushirikiana na serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha kua zoezi la Sensa lina kamilika. Bw. Paul Makanza aliendelea kusema kuwa wameshirikiana na Serikali katika vikao kadhaa na kuainisha maeneo saba ambayo sekta binafsi inaweza kuunga mkono serikali kwenye swala la Sensa.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni utoaji wa huduma, vifaa, utoaji elimu, usafiri, usafirishaji wa vifaa, utoaji wa matangazo na kuchangia mafuta ya magari. Alisema baadhi ya kampuni za simu zilianza kurusha jumbe fupifupi kwa wateja wao, vituo vya redio na televisheni navyo vilianza matangazo kuhamasisha jamii.

Ambapo, baadhi ya makampuni hayo leo yalipata kutambulika na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na kupewa tuzo maalum ya heshima ikiwa ni ishara ya kuthamini ushiriki wao kwenye zoezi la sensa 2022.

Makampuni yaliyopewa tuzo hio maalumu ni Azam Media, Stanbic Bank Tanzania, MIC Tanzania Plc (TIGO), Vodacom, Tanzania Mortgage Refinance Company Limited (TMRC), TUTUME Worldwide Limited, Waziri Mkuu pia alipokea ahadi toka makampuni mbalimbali ikiwemo CRDB na NORPLAN Tanzania.

Akiiongoza TPSF kwa Niaba ya Bodi, Bw. Makanza alitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio na hatua mnazochukua kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa Sekta Binafsi kufanya majukumu yake. Na alimshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuwapa sekta binafsi muda wake adhimu na pia kwa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika kuchangia shughuli za maendeleo ya nchi. Na kutoa wito kwa wadau wa sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kuchangia na kushirikiana na serikali katika zoezi muhimu la sensa ya watu na makazi.

Kwa upande wake Mhe. Kassim Majaliwa aliishukuru TPSF kwa ushiriki wa sekta binafsi katika kuchangia rasilimali fedha na rasilimali nyingine zitakazotumika kwenye Sensa ya Watu na Makazi 2022 na kutoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kuchangia kwani sensa ni jukumu la kila mmoja, hivyo ni vizuri tukalibeba kama Taifa.

Akizungumzia umuhimu wa sensa kwa wafanyabiashara Waziri Mkuu amesema: “Kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara, sensa ni chanzo cha msingi cha taarifa za kidemografia na ukuaji wa soko la bidhaa na huduma katika nchi zote duniani. Takwimu zote za biashara zinahitaji takwimu za idadi ya watu kama kigezo cha msingi cha kufanya maamuzi ya uwekezaji, uzalishaji na biashara.”

Katika mkutano huu Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. George Simbachawene pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. John Jingu, na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Bi. Anne Makinda na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Zanzibar, Mh. Mohammed Haji Hamza.