SEKTA BINAFSI TANZANIA YACHANGAMKIA FURSA ZA MAONESHO YA DUBAI EXPO 2020.

Dar es Salaam, 26 Oktoba 2021

Taasisi  ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kuona umuhimu wa ukuzaji wa Biashara Tanzania na fursa za kiuchumi zilizopo kwenye Masoko ya kimataifa, TPSF kupitia Mkurugenzi Mtendaji Bw. Francis Nanai iliungana na wajumbe kutoka Tanzania wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dotto James. Wajumbe hao walitembelea mabanda tofauti katika Maonesho ya Kibiashara ya Dubai EXPO 2020  yanayoendelea huko Umoja wa Falme za Kiarabu, Jijini Dubai.

“EXPO” ni maonesho ya Dunia yanayosimamiwa na Shirika la Kimataifa lijulikanalo kama Bureau of International Exhibition (BIE) lenye nchi wanachama 195. Maonesho haya hufanyika kila baada ya miaka mitano na yanadumu kwa miezi sita. Awali maonesho hayo yalipangwa kufanyika kuanzia tarehe 01 Oktoba 2020 hadi 31 Machi, 2021 lakini kutokana na changamoto ya Ugonjwa wa Uviko 19 yalisogezwa mbele na yameanza rasmi tarehe 01 Oktoba, 2021 na yanatarajiwa kumalizika mwakani tarehe 31 Machi, 2022.

Ujumbe kutoka Tanzania uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe.Dotto James na mwenyeji wao ambaye ni Balozi wa Tanzania Nchi za falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Mohammed Mtonga pia ni Kamishna Jenerali wa Maonesho ya Dubai Expo 2020. Pia waliambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Tanzania (TNBC) Dkt. Godwill Wanga pamoja na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Dubai Expo 2020, Bi. Getrude Ng`weshemiwa TanTrade.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 191 zinazoshiriki Maonesho hayo. Ushiriki wa Nchi yetu unaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda- Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashra Tanzania (TanTrade). Aidha, tunashiriki kupitia Ubalozi wetu uliopo Abu Dhabi pamoja na wadau wengine wa Sekta Binafsi.

Kaulimbiu ya maonesho haya ni “Connecting Minds, Creating the Future”, inayolenga kuzileta nchi zote duniani pamoja katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia kwa sasa katika sekta ya biashara, kilimo, nishati, madini, uchukuzi, viwanda, teknolojia, utalii, elimu, afya na huduma za kijamii. Tanzania inashiriki katika eneo la “Mobility” lenye kaulimbiu ndogo isemayo “Connectivity, Tanzania Ready for Take Off” ambayo inaonesha juhudi za serikali katika kuitangaza Tanzania kibiashara na kiuwekezaji.

“Ujumbe kutoka Tanzania tulifanya matembezi mahususi ili kujionea jinsi maonesho haya yanavyofanyika ili kuweza kujifunza na kuleta ujumbe sahihi kwa wafanyabiashara Wakitanzania ili kuwapa hamasa kuweza kushiriki". Amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Francis Nanai.

Pamoja na mambo mengine, Tanzania inatangaza miradi ya kimkakati kama vile mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Kisasa (SGR), Upanuzi wa Bandari ya Dar-es-Salaam, Ujenzi wa Viwanja vya Ndege na uimarishaji wa usafiri wa anga. Miradi hiyo ni kivutio na kichocheo cha ukuaji wa biashara na uwekezaji hususani katika sekta ya kilimo na viwanda.

Kadhalika, nchi yetu inatarajia kutumia fursa hii kubwa kutangaza na kutafuta masoko ya uhakika na endelevu ya bidha zitokanazo na mazao ya kimkakati kama vile kahawa, korosho, chai, mkonge, karafuu, viungo. Bidhaa za ngozi pamoja na bidhaa nyingie zinazokidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

Baadhi ya Fursa alizoelezea Bw. Francis Nanai ni pamoja na;

1. Kuona na kujifunza ni namna gani wafanyabiashara kutoka nchi zingine wanavyofanya shughuli zao.

2. Kuonesha bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania.

3. Kushiriki Mikutano ya Kibiashara (B2B) inayojikita katika sekta ya uwekezaji wa miundombinu, teknolojia, mipango miji na vijiji, elimu, ufundi na ubunifu, mifumo ya ufundishaji, fursa za utalii (hoteli, uwindaji, michezo, mazingira na fukwe), usafirishaji na mawasiliano, kilimo, uongezaji thamani wa mazao. N.k

Pia unaweza kupata taarifa zaidi kwa kupakua app ya Expo 2020 Business www.expo2020dubai.com  ambayo unaweza kujisajili Kwa kulipia Dola 3 za Kimarekani na hii ni kwa wale wenye simu janja (Android pamoja na IOS).

Bw. Francis Nanai amesisitiza kutumia fursa ya mifumo ya kidijitali kuweza kuonesha bidhaa tofauti kwenye maonesho ya Dubai Expo 2020 kwa kuchukua video zenye viwango vya juu na picha mnato zenye maelezo ya kujitosheleza kuhusu bidhaa husika na kutuma TanTrade (kwa maelekezo yao). Pia ametilia mkazo kuwa kila mfanyabiashara aweke “QR Codes” kwenye bidhaa zake.

Mwisho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua nchi kiuchumi,na sasa kazi inabaki kwetu watu wa sekta binafsi kutoa mchango wetu. Ili kufanikisha azma hii, niwaombe watanzania wote tumsaidie Mhe. Rais kwa kuchangamkia hizi fursa na kushiriki kikamilifu na kutangaza biashara za Tanzania nje ya nchi na pia kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwetu,kwani fursa kama ya Dubai Expo 2020 ni ufunguzi wa uchumi wa Tanzania.