SEKTA BINAFSI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTEKELEZA MIRADI YA KUKUZA UCHUMI

Tarehe 6 Oktoba, 2022 Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ilishiriki kwenye ufunguzi wa maonesho ya tatu ya wiki ya uwekezaji na biashara Pwani, ikiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Taasisi Ya Sekta Binafsi anayeongoza Kongani ya huduma Bw. Octavian Mshiu. Mgeni rasmi wa maonesho haya alikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza wakati wa kutoa salamu za sekta binafsi kwenye uzinduzi wa maonesho hayo Bw. Mshiu aliipongeza serikali kwa kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa katika Mkoa wa Pwani iliyo katikati ya ukanda wa Pwani wa nchi yetu, ambapo miradi imekuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo la Pwani.

Baadhi ya miradi hiyo ni mradi wa SGR wenye vituo katika kata ya Soga, Ruvu na Kwala, utekelezaji na ujenzi wa bandari kavu iliyopo Kwala pia uendelezwaji wa kongano ya viwanda TAMCO.

“Ni Faraja kujua kuwa kuna zaidi ya ekari 8,000 za ardhi ambazo zimetengwa maalum kwa fursa za uwekezaji hivyo kuufanya Mkoa wa Pwani kuwakilisha fursa za kipekee kwa Sekta Binafsi kwenye maeneo ya uwekezaji katika viwanda vikubwa na vya kati, biashara ya makazi, pamoja na uwekezaji wa makampuni ya usambazaji yanayotaka kupata masoko ya thamani ya juu nchini Tanzania na nchi Jirani.” Aliongezea Bw. Octavian

Vilevile mgeni rasmi wa hafla hiyo Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa kauli mbiu ya maonesho hayo inayosema “Pwani Sehemu Sahihi ya Uwekezaji" inaendana na hali ya Pwani ya sasa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na inaendana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuvutia wawekezaji wengi kuja nchini.

Hata hivyo, Mhe. Kikwete alisitiza kuwa uchumi unakuwa kwa uwekezaji na kusema, “Ukisema unataka uchumi ukuwe kwa asilimia saba ni lazima uboreshe mazingira mazuri ya biashara.

Kadhalika, wafadhili wakuu wa maonesho haya, kampuni ya Sino Tani imepewa ekari 2500 za kujenga kongani (industrial park), zenye viwanda 400 itakayoleta ajira ya moja kwa moja kwa watu laki moja na ajira zisizo za moja kwa moja laki tatu.

TPSF imeahidi kuendelea kuhamasisha Ushiriki wa Sekta Binafsi katika uwekezaji katika Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Kilimo, Miundombinu, Biashara na Huduma kama inavyoelekezwa na Mipango ya Maendeleo ya Mkoa wa Pwani na Taifa (FYDP III, Dira 2025, 2030).

Kwenye uzinduzi huu Bw. Mshiu aliambatana Mjumbe mwenzake wa bodi ya TPSF anayeongoza kongani ya Makampuni makubwa , ambaye pia ni Mbunge na Mfanyabiashara na Mwekezaji Mhe. Sylivestry Koka (MB).