TAASISI YA SEKTA BINAFSI TANZANIA (TPSF) NA TRC WAFANYA KONGAMANO LA KWANZA KUJADILI FURSA KATIKA MRADI WA SGR

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania kwa kushirikiana na TRC wamefanya kongamano la kwanza la wadau wa sekta binafsi ili kujadili fursa katika mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa – SGR kipande cha mwanza – isaka katika ukumbi wa benki kuu ya tanzania jijini mwanza tarehe 30 January 2021.


Lengo la mkutano huo ni kuandaa mpango kazi wa ushirikishwaji wa sekta binafsi nchini katika mradi huo unaotarajia kuanza ujenzi wake hivi karibuni ambapo mkandarasi kutoka China kampuni ya China Civil Engineering Constructtion Corporation pamoja na China Railway Construction Company watatekeleza mradi huo.


Akielezea umuhimu wa Kongamano hilo Mwenyekiti wa TPSF Bi. Angelina Ngalula alisema kuwa kongamano hilo linalenga kuangazia masuala makuu matano ambayo ni:

  1. Watanzania kufahamu maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kampuni za kitanzania ndogo ndogo pamoja na kubwa.
  2. Ujuzi unaohitajika au uwezo katika kila eneo.
  3. Mitaji ya kuendeshea kazi kwa watoa huduma na wakandarasi watakaopata fursa ya kutoa huduma katika mradi huu.
  4. Taasisi za fedha za ndani zilivyojipanga kuwadhamini watoa huduma kwa maana ya mitaji ya kuendesha kazi.
  5. Vigezo vya kuwapata watoa huduma wenye weledi

“Kongamano hili lina lengo la kutengeneza mfumo wa pamoja kati ya TRC, Sekta Binafsi na Mkandarasi wa namna watanzania watakavyoshiriki na kufaidika na mradi huu mkubwa wa kimkakati,”alisema Bi. Ngalula.


Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. John Mongela ambapo wadau kadhaa wa sekta binafsi wakiwemo wasafirishaji wa mizigo, wakandarasi, wavuvi, kampuni za uzalishaji, viwanda na wajasiriamali wadogo wadogo walihudhuria kongamano hilo.


Wadau wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na bodi ya usajili wahandisi Nchini, Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi na bodi ya usajili wakandarasi nchini.


Mkurugenzi mkuu wa wa shirika la reli Tanzania Bw. Massanja Kadogosa amesema kuwa kongamano hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt John Pombe Magufuli kuhakikisha sekta binafsi zinashirikishwa katika miradi mikubwa ya kimkakati ili kukidhi makubaliano ya kimkataba katika miradi na kuleta manufaa kwa taifa.


Wadau walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata majibu pia waliweza kutoa maoni juu ya upatikanaji wa taarifa za fursa za kibiashara katika mradi huo. Kongamano hili linakuwa la kwanza kufanyika nchini kwa lengo la kujadili namna sekta binafsi zitakavyoshiriki katika miradi ya kimkakati nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *