Leo tarehe 3 Oktoba 2022, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) imeandaa kikao cha wadau kuzungumzia mwongozo wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Kikao hiki kimeongozwa na kamisaa wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Mhe. Anne Makinda akiambatana na kamisaa wa sensa ya watu na makazi Zanzibar Mhe. Balozi Mohd Haji Hamza.

Kama mnavyofahamu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu ilifanya Sensa ya Watu na Makazi na ya majengo. TPSF kama mshirika mkuu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania iliunga mkono mpango wa Serikali wa kufanya Sensa hiyo kwa ushiriki wa kikamilifu wa sekta binafsi.
Hivyo basi, kikao cha leo kimewakutanisha tena serikali na sekta binafsi kujadiliana mwongozo wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi Pamoja na sensa ya majengo, 2022.

Kati ya hoja zilizowasilishwa na wadau mbalimbali wa sekta binafsi ni pamoja na kuitaka serikali;
1/Kuunganisha mifumo ya utoaji taarifa
2/Kujikita kwenye uchunguzi wa soko la ajira na ujuzi unao hitajika kukidhi majitaji ya soko hilo
3/Kuongeza nguvu kwenye vyuo vya ufundi
4/ Kuweka data za sensa kwenye mfumo ambao utatumika na wawekezaji kama fursa

Mhe. Anne Makinda alishukuru ushiriki wa sekta binafsi kwa kutoa maoni yenye tija na kuomba ushirikiano uwe endelevu ili kupata mwongozo mzuri.

Mwisho, Wadau wa sekta binafsi wameshukuru kushirikishwa katika majadiliano haya, na kutuma salamu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kupongeza Jamhuri ya Muungano kwa kazi nzuri waliofanya kipindi cha sensa. Sekta binafsi pia imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika katika kuboresha miongozo mbalimbali.